“Bora elimu badala ya elimu bora” yakwamisha watoto Afrika Mashariki- Ripoti

27 Septemba 2017

Elimu ya msingi na sekondari inayotolewa katika nchi za kipato cha chini na kati ulimwenguni inakwamisha mamilioni ya watoto kufanikiwa kwenye maisha yao ya baadaye.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Benki ya Dunia kuhusu Kujifunza ili kunufaika na elimu ambayo imesema hata baada ya kusoma miaka kadhaa shule, watoto bado hawajui kusoma, kuandika na hata kufanya hesabu rahisi.

Mmoja wa wachumi waandamizi wa Benki ya Dunia na wahusika wa ripoti hiyo  Deon Filmer ametolea mfano nchi za Kenya, Tanzania na Uganda watoto wa darasa la tatu walipatiwa sentensi rahisi ya lugha ya kiingereza lakini hawakuelewa maana yake.

Ametaja sababu mbili za mtoto kwenda shule lakini kutoweza kujifunza chochote kuwa ni mosi..

(Sauti ya Deon)

“Wanafunzi wanafika shule bila ya kuwa tayari kujifunza au bila ya msingi thabiti wanaohitaji, na pili ni walimu kutokuwa na motisha au stadi au hawajajiandaa.”

Naye  Halsey Rogers amesema ripoti inataka uwekezaji usiishie tu kama ilivyo sasa katika kuandikisha watoto wengi shuleni bali pia..

(Sauti ya Halsey)

“Jinsi ya kuhakikisha kwamba fedha inatumika vizuri kufanikisha lengo la elimu kwa wote; elimu kwa watoto na vijana. Hii ikimaaniha kwamba kuangazia zaidi katika kuangalia matokeo ya kujifunza tofauti na ilivyokuwa hapo awali.”

Benki ya dunia imesema iwapo elimu itatolewa vizuri, itakidhi matarajio ya vijana ya kupata ajira bora, kipato bora, afya bora na ahta maisha bila umaskini.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter