Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DPRK yafanya jaribio la nyuklia, Guterres, IAEA walaani

DPRK yafanya jaribio la nyuklia, Guterres, IAEA walaani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali jaribio la nyuklia lililofanywa leo na Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK.

Jaribio hilo lililofanyiwa chini ya ardhi, ni la sita tangu mwaka 2006 na linafuatia majaribio mengine mawili ya aina hiyo yaliyofanywa mwaka jana.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Katibu Mkuu akisema kuwa kitendo hicho cha DPRK ni ukiukwaji mkubwa wa wajibu wa nchi hiyo kimataifa na kinadumaza jitihada za kimataifa za kuondoka na uenezaji na usambazaji wa silaha.

Bwana Guterres amesema DPRK pia inaendelea kukiuka maadili ya kimataifa dhidi ya majaribio ya nyuklia akisema anafuatilia kwa karibu hali ya sasa huku akishauriana na pande husika.

Nalo shirika la kimataifa la nishati ya atomiki, IAEA limetoa taarifa likisema linafuatilia kwa karibu mpango wa nyuklia wa DPRK na liko tayari kuchangia katika kusaka kwa amani suluhu ya suala hilo.