Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Polisi Somalia wanolewa kuhusu ukatili wa kingono

Polisi Somalia wanolewa kuhusu ukatili wa kingono

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa usaidizi nchini Somalia, UNSOM unawapatia polisi nchini humo mafunzo kuhusu jinsi ukatili wa kingono unavyoweza kuzua mizozo na kuotesha mizizi ukatili kwenye jamii.

Mafunzo hayo yanatolewa kupitia warsha ya siku tatu kwa kushirikiana na Wizara ya wanawake na haki za binadamu yataongeza ufahamu wa polisi kuhusu hatari za ukatili wa kingono na mizozo kwenye amani na usalama.

Charles Muwunga Mwebe ni kiongozi wa jopo la haki za binadamu la UNSOM mjini Baidoa, jimbo la Kusini-Magharibi nchini Somalia.

(Sauti ya Charles)

 “Police wana wajibu wa kuendeleza na kulinda haki za binadamu. Lakni inapokuja suala la wanawake, tunahisi kwamba wana wajibu wa kuwalinda popote pale walipo; iwe ni kwenye kambi za wakimbizi wa ndani, majumbani au pahala pa kazi. Kwa hiyo tunajaribu kuwafundisha na kujenga uwezo wao, jambo ambalo ni sehemu ya jukumu letu.

image
Nadifo Armey Abdullahi, Waziri wa masuala ya wanawake na haki za binadamu jimbo la Kusini-Magharibi . (Picha:UNifeed-Video Capture)
Kwa upande wake Nadifo Armey Abdullahi, Waziri wa masuala ya wanawake na haki za binadamu jimbo la Kusini-Magharibi amesema..

(Sauti ya Nadifo)

“Leo tuko kwenye mafunzo ya UNSOM yakijikita kwenye haki za binadamu na jinsi polisi wanaweza kushughulikia wahanga; wawe wa ukatili wa kingono au watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu ambao hawawezi kupata elimu. Mafunzo pia yanahusisha jinsi polisi wanaweza kutatua masuala katika jamii.”

Maafisa polisi 54 wanaoshiriki mafunzo haya watapatiwa mafunzo pia kuhusu haki za binadamu na ulinzi wa uhuru wa raia miongoni mwa jamii zilizo kwenye matatizo.