Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vikwazo vya kusafiri Cuba vitaathiri uchumi wa Marekani

Vikwazo vya kusafiri Cuba vitaathiri uchumi wa Marekani

Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani, UNWTO limelaani vikali uamuzi wa utawala wa Marekani kurejesha vikwazo vya kusafiri nchini Cuba.

UNWTO imesema hatua hii ni shambulio kubwa la uhuru wa kusafiri na inarudisha nyuma uhuru huo, na ingawa litaathiri utalii wa Cuba kwa kiasi, litaathiri zaidi uchumi na uwepo wa kazi nchini Marekani, kwani mashirika mengi ya Marekani yameanza kuwekeza na kufanya biashara na nchi hiyo kwa matumaini ya ongezeko la utalii.

UNWTO imesema utalii ni moja ya vigezo muhimu vya uchumi nchini Cuba, vyenye kuleta kipato kwa wengi, pamoja na kuvutia uwekezaji kutoka nje, na hilo litaendelea, lakini ni nchi zingine ambazo zitaendelea kunufaika.

Mwaka 2016 baada ya vikwazo hivyo kuondolewa, Cuba ilipokea watalii zaidi ya milioni 4, ongezeko la zaidi ya milioni moja katika kipindi cha miaka mitano tu.