Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano watakiwa kukamilisha uchunguzi wa kifo cha Hammarskjöld

Ushirikiano watakiwa kukamilisha uchunguzi wa kifo cha Hammarskjöld

Wakati uchunguzi wa chanzo cha ajali iliyosababisha kifo cha Katibu Mkuu wa zamani Dag Hammarskjöld mwaka 1961 ukiwa unaendelea, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametaka nchi wanachama kumpatia ushirikiano wa kutosha Mohammed Othman, ambaye anaongoza jopo la watu mashuhuri la kuchunguza kifo hicho.

Stephane Dujarric ambaye ni msemaji wa Umoja wa Mataifa amewaeleza waandishi wa habari kuwa Bwana Guterres ameazimia kuendeleza jukumu hilo la uchunguzi kuhakikisha ukweli unapatikana.

Kwa mujibu wa Dujarric, Bwana Othman ambaye Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, wiki iliyopita alikuwa na mashauriano na wanachama wa Umoja wa Mataifa akiwasihi wawasilishe taarifa zozote zinazoweza kuangazia hatua za mwisho za kuanguka kwa ndege iliyokuwa imemchukua hayati Hammarskjöld huko karibu na Ndola Zambia usiku wa kuamkia tarehe 18 Septemba mwaka 1961.

Amesema ushirikiano zaidi unatakiwa kutoka nchi wanachama ili kuweza kuachia taarifa ambazo bado ni za siri au kupata ruhusa ya kuangalia taarifa ambazo sasa ni za zaidi ya miaka 55.