UM watoa wito wa kuachiliwa Wayezidi wanaoshikiliwa na Daesh

19 Aprili 2017

Katika kuadhimisha mwaka mpya kwa jamii ya Wayezidi nchini Iraq , mwakilishi maalumu wa Umoja wa mataifa nchini humo Ján Kubiš, amewatakia kila la heri na kutoa wito wa kuachiliwa huru watu wa jamii ya Yezidi wanaoshikiliwa na kundi la kigaidi la Daesh.

Amesema wakati jamii hiyo ikisherehekea wakati huu muhimu , pia ni fursa ya kuwakumbuka waliopoteza maisha kutokana na uasi wa Daesh, huku akichagiza juhudi za kila aina kuhakikisha wanawake na watoto wanaoshikiliwa na kufanywa watumwa na kundi hilo wanaachiliwa huru.

Bwana Kubiš amesema kulishinda kundi hilo katika mapambano kwenye eneo la Ninewah kutahakikisha Wayezidi walio wachache ambao kundi hilo limewaweka katika kampeni ya mauaji , wanaishi wa amani na usalama siku za usoni.

Hivyo ameongeza kuwa ana matumaini madhila yao yatakwisha na Iraq iliyokombolewa itakumbatia jamii zote kwa amani na utangamano.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter