IAEA bado ina hofu kuhusu DPRK

IAEA bado ina hofu kuhusu DPRK

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kimataifa la nishati ya atomiki, IAEA, Dkt. Yukiya Amano ameseam bado ana wasiwasi mkubwa kuhusu mpango wa nyuklia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK wakati huu ambapo vyombo vya habari vinaripoti kuwa nchi hiyo siku ya jumapili imefyatua makombora manne ya masafa marefu.

Akihutubia mkutano wa bodi ya magavana wa shirika hilo ambao hukutana mara tano kwa mwaka huko Vienna, Austria, Dkt. Amano amesema kinachosikitisha zaidi DPRK haijaonyesha dalili yoyote ya kwamba iko tayari kuzingatia maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufuatia majaribio yake mawili ya nyuklia mwaka jana.

Kwa mantiki hiyo, mkuu huyo wa IAEA ameitaka DPRK kuzingatia kwa ukamilifu maazimio hayo na kutoa ushirikiano na hatimaye kupatia suluhu masuala kadhaa ikiwemo yale yaliyoibuka katika kipindi ambacho wakaguzi wa shirika hili hawajatembelea nchi hiyo.

Amesema IAEA inasalia tayari kutekeleza dhima muhimu katika kukagua na kuthibitisha mpango wa nyuklia wa nchi hiyo.