Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchafuzi wa hewa huua watoto, jihadhari: WHO

Uchafuzi wa hewa huua watoto, jihadhari: WHO

Kama ulifikiri magonjwa ndio sababu pekee ya vifo kwa watoto chini ya miaka mitano, sivyo! Mazingira hususani uchafuzi wa hewa ndani au nje ya nyumba , moshi umpatao asiyevuta tumbaku, ni mongoni mwa sababu ya kifo cha mtoto mmoja kati ya watano limesema shirika la afya ulimwenguni WHO. Amina Hassan na maelezo kamili.

( TAARIFA YA AMINA)

Katika ripoti zake mbili mpya, ya kwanza ikiitwa Kurithi dunia endelevu: Atlasi ya afya ya watoto na mazingira, inasema kuwa kwa asilimia kubwa ya vyanzo vya vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, ambavyo ni kuharisha, malaria na vichomi vikali yaani pneumonia yanazuilika kwa kupunguza athari za mazingira kama maji safi na salama na mafuta ya kupikia.

Ukuaji wa viungo vya watoto na mfumo wa kinga, miili midogo na njia za kupumua husababisha kundi hili kuwa katika hatari ya uchafu wa hewa na maji, imesema ripoti hiyo.

Ripoti ya pili yenye maudhui hayo iitwayo Usichafue mustakabali wangu! Madhara ya mazingira kwa afya za watoto, inaainisha takwimu za madhara ya mazingira kwa watoto, mathalani inasema kote duniani asilimia 11 hadi 14 ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kwa sasa wanaripotiwa kuwa na dalili za pumu.

Maria Neira, ni Mkurugenzi wa WHO idara ya afya ya umma,mazingira na jamii.

( Sauti Maria)

‘‘Moja ya hatua muhimu za kuchukua ni kupata mafuta masafi. Kama unavyofahamu karibu nusu ya idadi ya watu duniani wanatumia mafuta machafu, iwe kupikia, kupasha chakula au kwa ajili ya mwanga majumbani. Hii huathiri zaidi akina mama na watoto ambao huambatana nao. Kwa hiyo ikiwa tutaboresha usafi au kupata nishati salama majumbani, itakuwa na manufaa makubwa kwa watoto.''