Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mogadishu kimya, kuelekea uchaguzi wa rais Jumatano

Mogadishu kimya, kuelekea uchaguzi wa rais Jumatano

Kuelekea uchaguzi wa Rais wa Somalia kesho Jumatano, ukimya umetawala kwenye mji mkuu Mogadishu, huku wanaotakiwa kutembea kwenye mji huo ni wale wanaohusika na mchakato wa uchaguzi.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Michael Keating ameiambia radio ya Umoja wa Mataifa kuwa miongoni mwao ni wabunge, wagombea 23 wa Urais, vikosi vya usalama na kamati ya maandalizi ya uchaguzi.

Ametaja wengine ni kamati ya maadili inayojumuisha kundi la wasomali ambao kazi yao ni kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanyika salama.

Mathalani wanatoa maelekezo jinsi ya kutumia simu za rununu, na kwamba watu hawapaswi kubeba silaha na maeneo ya kuegesha maghari.

Bwana Keating amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake unasaidia mamlaka za Somalia kuandaa eneo la kupigia kura ambalo limehamishiwa uwanja wa ndege wa Mogadishu.

Watakaopiga kura ni wabunge 329 waliochaguliwa na wananchi katika mchakato wa uchaguzi uliochukua miezi 18.