Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafunzo yafanyika kunasua watoto vitani Somalia

Mafunzo yafanyika kunasua watoto vitani Somalia

Ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM na kikosi cha taifa la Somalia SNA wanachukua hatua za kuzuia utumikishaji watoto jeshini.

Hatua hii imekuja kufuatia ongezeko la matukio hayo yanayotajwa kuwa yanatishia usalama katika pembe ya Afrika.

Taarifa ya AMISOM imesema hatua hizo zinahusisha mafunzo ya siku 10 kwa wakufunzi kutoka serikali ya Somalia na maafisa wa AMISOM, mafunzo ambayo yatawapatia stadi za kunasua watoto kutoka vikundi vya kijeshi nchini Somalia.

Akizungumzia kwenye mafunzo hayo yanayofanyika Nairobi, Kenya, Naibu Mwakilishi maalum wa Muungano wa Afrika nchini Somalia Lydia Wanyoto amepongeza mafunzo hayo akisema ni hatua muhimu ya kunasua watoto wa Somalia kutoka kwenye mapigano.

Mafunzo yanatolewa na walimu kutoka kikundi cha Uingereza cha usaidizi wa amani Afrika Mashariki na mpango wa Dallaire.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 70 ya watoto kwenye mizozo huko Somalia wanatumikishwa na kikundi cha kigaidi cha Al-Shabaab.