Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kilichotokea Gambia ni ushindi kwa Afrika na dunia: Chambas

Kilichotokea Gambia ni ushindi kwa Afrika na dunia: Chambas

Waafrika wametekeleza jukumu muhimu la kukuza demokrasia, amani na usalama na kisha kukabidhi madaraka kwa amani nchini Gambia amesema Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ukanda wa Afrika Magharibi Mohamed Ibn Chambas.

Katika mahojiano maalum kwa njia ya simu na redio ya Umoja wa Mataifa, Bwana Chambas ambaye alisafiri na Rais mpya wa Gambia Adama Barrow kutoka Senegal alikoapishwa hadi Banjul mji mkuu wa Gambia, amesema jumuiya ya uchumi Afrika Magharibi ECOWAS imetuma ujumbe kwa dunia kuhusu mabadiliko chanya katika bara hilo hususani katika sekta ya demokrasia.

Amesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kujifunza kuwa.

(Sauti Chambas)

‘‘Huu ni ushahidi tosha wa matumizi ya  diplomasia ya uzuiaji, tulifanya kila  kitu pamoja, Umoja wa Mataifa na wadau wengine hususani wale wa kikanda, kuzuia Gambia kutumbukia katika machafuko kwenye bara hilo.’’

Aliyekuwa Rais wa Gambia Yahya Jammeh alikataa kutoka madarakani licha ya kushindwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, hatua iliyolazimu jumuiya ya kimataifa ikiongozwa na ECOWAS kumlazimisha kukabidhi madaraka kwa Rais mteule Barrow.