Skip to main content

Walinda amani Haiti wamepatiwa chanjo dhidi ya Kipindupindu

Walinda amani Haiti wamepatiwa chanjo dhidi ya Kipindupindu

Umoja wa Mataifa umesema polisi wote wanaolinda amani nchini Haiti ambao walikuwa bado hawajapatiwa chanjo dhidi ya Kipindupindu kabla ya kuwasili nchini humo sasa wameshapatiwa. Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema wamepatiwa chanjo ya kwanza na taratibu zinaendelea ili wapatiwe chanjo ya pili kama njia ya kudhibiti kuenea kwa Kipindupindu ambacho kimesababisha machungu miongoni mwa wananchi wa Haiti tangu mlipuko wake Oktoba 2010.

(Sauti ya Dujarric)

“Chanjo dhidi ya kipindupindu ni lazima kwa walinda amani wote wanaopelekwa kwenye operesheni za ulinzi wa amani na ni wajibu wa nchi wanachama kuhakikisha wafanyakazi hao wanapatiwa chanjo hiyo kabla ya kwenda eneo la kazi. Iwapo walinda amani wanawasili kwenye operesheni bila ya kuwa wamepatiwa chanjo zinazotakiwa, ofisi husika inapaswa kuchukua hatua kuwapatia.”

Amesema gharama zitokanazo na walinda amani kupatiwa chanjo husika mara baada ya kuwasili eneo la tukio hukatwa kutoka nchi ambako askari hao wanatoka.

Mwezi Disemba mwaka jana Umoja wa Mataifa uliomba radhi kutokana na jinsi ulivyoshughulikia tatizo la kipindupindu nchini humo.