Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Harakati zaendelea kutekeleza mkataba wa amani Colombia-Arnault

Harakati zaendelea kutekeleza mkataba wa amani Colombia-Arnault

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Colombia, Jean Arnault amesema utekelezaji wa mkataba wa amani kati ya serikali na kikundi cha FARC unaendelea ingawa kuna changamoto.

Akihutubia Baraza la Usalama hii leo, Bwana Arnault ametolea mfano kipengele cha kujumuisha uraiani wapiganaji wa FARC kinachoenda sambamba na usalimishaji silaha, akisema kinakwamishwa na kushamiri kwa shughuli haramu za kiuchumi kwenye maeneo yaliyokuwa na mapigano.

Amesema tarehe 20 mwezi uliopita baraza la kitaifa la ujumuishaji wapiganaji hao lilianzishwa na limeshakuwa na vikao vinne vinavyoangazia mpango wa kuwajumuisha uraiani wapiganaji waliosamehewa.

Hata hivyo amesema..

(Sauti ya Arnault)

"Kwa bahati mbaya kunasalia kutokuelewana kuhusu masuala ya watoto,ambayo tunaamini litatatuliwa karibuni."

Kuhusu suala la makazi kwa wapiganaji hayo Bwana Arnault ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Colombia, amesema..

(Sauti ya Arnault)

"Hadi sasa, ujenzi umeanza katika theluthi moja ya maeneo , maandalizi yanaendelea katika theluthi nyingine, wakati yaliyosalia yanaendelea kukabiliana na ugumu. Juma lililopita Rais Santos alitathimini hatua iliyofikiwa wakati wa ziara ambamo niliambatana naye katika moja ya maeneo kusini mwa Colombia.  Alitoa maagizo maalum ya kutatau vikwazo vinavyosalia na kuongeza juhudi maradufu ili kuwezesha kambi 26 kuwa tayari mapema zaidi."