Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuzo ya amani ya Nobel 2016 yaenda kwa Rais wa Colombia

Tuzo ya amani ya Nobel 2016 yaenda kwa Rais wa Colombia

Rais Juan Manuel Santos wa Colombia ameshinda tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka huu wa 2016. Flora Nducha na maelezo zaidi..

(Sauti ya Flora)

Nats..

 Kaci Kullmann Five, mwenyekiti wa kamati ya Nobel akimtangaza hii leo Rais Juan Manuel Santos wa Colombia kuwa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka 2016, na msingi wa uamuzi wao ni kufanikisha kwake mkataba wa amani na kikundi cha FARC-EP uliomaliza zaidi ya miongo mitano ya vita vya wenyewe kwa wenyewe..

Kufuatia hatua hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akizungumza na wanahabari huko Hamburg, Ujerumani amesema tuzo hii imekuja wakati muhimu ambapo wananchi wa Colombia wanahitaji matumaini na kutiwa moyo kuhusu mkataba wa amani, mkataba ambao kura ya maoni ya tarehe Pili mwezi huu iliupinga.

Hivyo amesema…

(Sauti ya Ban)

“Ujumbe wa tuzo hii uko wazi, wananchi wa Colombia wametoka mbali kuamua kurudi nyuma hivi sasa. Mchakato wa amani umekuwa na utaendelea kuwa msukumo kwa dunia ambayo tunaihitaji hivi sasa.”

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Colombia vilisababisha vifo vya zaidi ya watu 220,000 huku wananchi zaidi ya milioni sita wakikimbia makazi yao.