Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hukumu ya kifo isitumike kama njia ya kuzuia ugaidi:UM

Hukumu ya kifo isitumike kama njia ya kuzuia ugaidi:UM

Wakizungumza kuelekea siku ya kimataifa ya kupinga hukumu ya kifo hapo Jumatatu Oktoba 10, wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, wamezikumbusha serikali kote duniani, kwamba hukumu ya kifo haipaswi kutumika kuzuia ugaidi, na mara nyingi ni ukiukwaji wa sheria.

Wawakilishi hao maalumu, Agnes Callamard wa kuhusu mauaji ya kiholela, Juan E. Méndez wa kuhusu utesaji, na Ben Emmerson, wa kuhusu haki za binadamu wakati wa kupambana na ugaidi, wamesisitiza kwamba tishio la ugaidi halihalalishi kukiuka viwango vya kimataifa vya kulinda haki za binadamu.

Wamesema kuna baadhi ya nchi ambazo zimeshambuliwa kigaidi au zinakabiliwa na tishio la ugaidi, hivi karibuni zimegeukia hukumu ya kifo katika jaribio la kupambana na vitendo vya kigaidi, ama kwa kupanua wigo wa makosa yanayopewa hukumu ya kifo, au wamerejea kunyonga watuhumiwa wenye makosa yanayohusiana na ugaidi baada ya miaka mingi kuachana na utekelezaji wa hukumu hiyo.

Wamesema hatua hizo zina shida hasa kwa nchi ambazo zilifuta hukumu ya kifo na kuirejea tena, kwani wanakwenda kinyume na mtazamo wa kimataifa unaochagiza kufutwa kwa hukumu ya kifo.

Mwaka 2015, hukumu ya kifo kwa makosa yanayoambatana na ugaidi ilitolewa kwa nchi 7 na unyongaji mkubwa ukifanyika Mashariki ya Kati na Afrika ya kaskazini.