Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Keating alaani mauaji ya mwandishi wa Radio Shabelle Somalia

Keating alaani mauaji ya mwandishi wa Radio Shabelle Somalia

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Michael Keating amelaani vikali mauaji ya mwandishi wa habari wa Radio Shabelle Abdiaziz Mohamed Ali yaliyofanyika jana na watu wasiojulikana mjini Moghadishu Somalia.

Mwandishi huyo na ripota mashuhuri , amekuwa mwandishi wa pili kuuawa kikatili mwaka huu. Jumla ya waandishi wa habari 31 wameuawa nchini Somalia tangu mwezi Agosti mwaka 2012 , kwa mujibu wa mpango wa umoja wa Mataifa nchini humo UNSOM kitengo cha ulinzi na haki za binadamu.

Bwa Keating amesema Ali alikuwa mwandishi mwenye ujuzi na utaalamu wa kutosha aliyekuwa akiripoti mikutano mbalimbali ya jumuiya ya kimataifa mjini Moghadishu, na kifo chake ni pigo kubwa kwa jumuiya ya tasnini ya habari nchini humo. Ametuma salamu za rambirambi kwa familia , jamaa na marafiki wa Ali.

UNSOM imetoa wito kwa serikali ya Somalia kuhakikisha wahusika wa uhalifu huo wa kikatili wanafikishwa mbele ya mkono wa sheria.