Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano makali yanaendelea Juba, watu zaidi ya 200 wapoteza maisha

Mapigano makali yanaendelea Juba, watu zaidi ya 200 wapoteza maisha

Mapigano makali yanaendelea mjini Juba Sudan Kusini huku duru zikisema mamia ya watu wamepoteza maisha. Grace Kaneiya na habari kamili

(TAARIFA YA GRACE)

Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa machafuko hayo yameathiri pia wakimbizi wa ndani walioko kwenye maskani ya Umoja wa Mataifa. Watu zaidi ya 200 wamearifiwa kuuawa, wengi kujeruhiwa wakiwemo walinda amani wa Umoja wa Mataifa. Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP linasema watu zaidi ya 10,000 wamekimbia wakiwemo 3000 waliokuwa wakipata hifadhi kwenye kituo cha shirika hilo.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa Jumapili limefanya kikao cha dharura kujadili hali hiyo. Rais wa Baraza balozi Koro Bessho ametuma salamu za rambirambi kwa familia za walinda amani waliouawa, huku Baraza likilaani vikali kuzuka upya kwa mapigano na mashambulizi dhidi ya raia na Umoja wa Mataifa.

Baraza limewataka viongozi hasimu Rais Salva Kiir na makamu wake wa kwanza wa Rais Riek Machar kufanya kila liwezekenalo kudhibiti vikosi vyao, kukomesha mapigano haraka na kuzuia ghasia zisisambae zaidi. Pia Baraza limezichagiza nchi katika kanda kuwa tayari kutoa vikosi vya ziada kwenda Sudan Kusini endapo itaamuriwa hivyo.