Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNSOM alaani shambulizi la kigaidi na mauaji ya waziri Mogadishu

Mkuu wa UNSOM alaani shambulizi la kigaidi na mauaji ya waziri Mogadishu

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu nchini Somalia, Michael Keating, amelaani vikali shambulizi la kigaidi mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya hoteli ya Naso Hablod kusini mwa Mogadishu, ambako watu 25 wameripotiwa kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Mmoja wa wahanga wa shambulizi hilo alikuwa Bwana Buri Mohamed Hamza, Waziri wa Mazingira katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

Bwana Keating amesema amechukizwa mno na shambulio hilo lililokatili maisha ya watu wengi, akiongeza kuwa kifo cha Waziri Hamza kinatia huzuni hata zaidi kwani alikuwa mtu mwenye hamasa kubwa katika kupigania mazingira nchini Somalia.

Kikundi cha kigaidi cha Al-Shabaab kimedai kutekeleza shambulizi hilo dhidi ya hoteli ya Naso Hablod, ambayo aghalabu hutumiwa na wanasiasa na watalii.