Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zeid aitaka Marekani kuchukua hatua madhubuti kudhibiti silaha

Zeid aitaka Marekani kuchukua hatua madhubuti kudhibiti silaha

Kufuatia mauaji ya watu 49 kwenye moja ya vilabu vya usiku jimboni Florida, yaliyofanywa na mtu mwenye silaha, kamishina mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein, ameitaka Marekani kutekeleza wajibu wake wa kulinda raia wake kutokana na mashambulizi ya kikatili yanayoweza kuzuilika, ambayo ni matokeo ya kutodhibiti silaha vya kutosha.

Zeid amesema ni vigumu kupata sababu inayohalalisha urahisi wa watu kununua silaha, ikiwemo za vita , licha ya kuwemo mashambulizi ya nyuma, historia ya uhalifu, matumizi ya mihadarati, ukatili majumbani na matatizo ya akili au uhusiano wa moja kwa moja na watu wenye itikadi kali wa ndani na wa kigeni.

Msemaji wa ofisi ya haki za binadamu, Rupert Colville amemnukuu Zeid akihoji ni kiwango gani zaidi cha mauaji kinahitajika, ili Marekani ipitishe sheria za kudhibiti silaha akitaja mauaji ya watoto wa shule, wafanyakazi, waumini, wamarekani weusi, na hata ya mwimbaji chipukizi Christina Grimmie na mwanasiasa Gabrielle Giffords.

Amehoji ni kwa nini raia popote waweze kumiliki silaha nzito nzito zilizotengenezwa kwa ajili ya kuua idadi kubwa ya watu.

Ameongeza kuwa propaganda zisizo na msingi zinaonyesha silaha hizo za moto zinaifanya jamii kuwa salama, lakini ukweli na ushahidi wote ni kinyume kabisa.