Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kaswende na VVU yafungashwa virago Thailand na Belarus

Kaswende na VVU yafungashwa virago Thailand na Belarus

Shirika la afya duniani, WHO limepongeza Thailand na Belarus kwa kuweza kutokomeza maambukizi ya virusi vya Ukimwi, VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, halikadhalika ugonjwa wa Kaswende ujulikanao pia kama Sekeneko.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Margaret Chan amesema ni jambo la kutia moyo kuona nchi hizo zikitokomeza maambukizi hayo akisema hatua za kuhakikisha watoto wanazaliwa na afya bora ni kuwapatia mwanzo mzuri wa maisha.

Wakati huo huo Dkt. Chan ameipongeza Armenia kwa kutokomeza maambukizi  ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto huku Moldova nayo ikiibuka kidedea kwa kutokomeza maambukizi ya Kaswende.

WHO imesema hatua hizo ni kiashiria kuwa dunia iko katika mwelekeo wa kuondokana na Ukimwi na kwamba kumaliza maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto, pamoja na Kaswende ni msingi wa kufikia lengo la dunia la kumaliza Ukimwi ifikapo mwaka 2030.

Mwaka 2014, WHO na wadau wake waliweka vigezo vya kuthibitisha kuwa nchi imetokomeza maambukizi ya magonjwa hayo mawili kupitia tathmini ya hali ya juu.

Mwaka jana Cuba ilikuwa nchi ya kwanza kuthibitishwa kutokomeza VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, halikadhalika Kaswende.