Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nuru yaonekana kwa watoto wanaotumikishwa vitani Colombia

Nuru yaonekana kwa watoto wanaotumikishwa vitani Colombia

Watoto wote wanaotumikshwa vitani kwenye kundi la waasi wa FARC-EP nchini Colombia wanatakiwa kujisalimisha na kurejeshwa kwenye jamii. Hii ni kwa mujibu wa mkataba wa makubaliano baina ya serikali ya Colombia na FARC uliosainiwa leo mjini Havana.

Akihudhuria utiaji saini huo, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto kwenye mizozo Leila Zerrougui amekaribisha hatua hiyo muhimu akisema itaweza kubadilisha maisha ya watoto wengi, ambao hawajawahi kushuhudia amani nchini mwao.

Bi Zerrougi amepongeza pande za mzozo na wadau wengine wakiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhdumia watoto UNICEF na mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Colombia kwa mchango wao katika kufikia makubialiano hayo.

UNICEF imesema watoto wote wenye umri wa chini ya miaka 15 wataanza kujisalimisha, na baada ya hao watafuata watoto wote wenye umri wa chini ya miaka 18. Akihojiwa na Redio ya Umoja wa Mataifa, Mwakilishi wa UNICEF Roberto de Bernardi amesema tayari watoto 6,000 wamejisalimisha kutoka kwa vikundi hivyo kwa kipindi cha miaka 15, na hivyo idadi nzima ya watoto wanaotumikishwa vitani hadi sasa inakadiriwa kuwa kubwa zaidi.

(SAUTI YA ROBERTO DE BERNARDI)

"Inamaanisha kwamba watoto hao wachukuliwe kwanza kama wahanga na sio wauaji. Ni muhimu sana kwamba kwenye taarifa iliyotolewa kwa pamoja suala hilo muhimu limekaririwa tena."