Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano la UNFPA kuhusu wanawake laanza mjini Copenhagen

Kongamano la UNFPA kuhusu wanawake laanza mjini Copenhagen

Kongamano kuhusu afya, haki na maslahi ya wanawake na wasichana, limeanza leo mjini Copenhagen, Denmark, likiwa ndilo kubwa zaidi katika kipindi cha mwongo mmoja, na moja ya makongamano ya kwanza kabisa tangu kuzinduliwa kwa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Kongamano hilo la Women Deliver, limeandaliwa na Shirika la Idadi ya Watu (UNFPA), na linazingatia jinsi malengo ya SDG yanavyohusiana na wanawake na wasichana, kwa kumulika hasa afya ya uzazi, na jinsi inavyoingiliana na usawa wa jinsia, elimu, mazingira, na maendeleo ya kiuchumi.

Kongamano hilo la Mei 16 hadi Mei 19 2016, linawaleta pamoja viongozi, wanaharakati, watunga sera, wanahabari, vijana, watafiti na viongozi kutoka sekta binafsi na mashirika ya kiraia, kuonyesha kinachoweza kutokea iwapo wanawake watazingatiwa katika juhudi za maendeleo.

Nana Kuo ni Meneja Mkuu wa mpango wa kila mwananake kila mtoto katika Umoja wa Mataifa.

(SAUTI NANA)

‘‘Hatutaweza kufanikisha SDGS ikiwa hatutawaweka wanawake katika kitovu cha malengo hayo. Kongamano linatoa fursa ya kubadilishana uzoefu na kufahamiana na wadau wengi hususani kutoka mashinani katika nchi. ‘’