Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban na Dlamini-Zuma wakaribisha uchaguzi wa amani Comoros

Ban na Dlamini-Zuma wakaribisha uchaguzi wa amani Comoros

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Muungano wa Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma, wamekaribisha kukamilishwa kwa amani awamu ya pili ya uchaguzi wa Rais wa Comoros na Gavana wa kisiwa cha Anjouan.

Viongozi hao wawili wamewapongeza watu wa Comoros kwa kushiriki awamu zote mbili za uchaguzi huo kwa njia ya amani, wakitoa heko kwa taasisi husika za kitaifa kwa kuandaa awamu ya pili ya uchaguzi kwa njia taratibu. Wameongeza kuwa taasisi hizo sasa zina wajibu muhimu wa kuhakikisha kuwa matokeo ya uchaguzi huo kweli yanadhihirisha matakwa ya watu wa Comoros.

Aidha, wamehimiza Mahakama ya Katiba itangaze matokeo ya mwisho kwa njia ya uwazi na mapema, na kutoa wito kwa wagombea wote kujidhibiti na kuonyesha hulka ya kuwajibika, pamoja na kujikita katika kufanya kazi kwa ajili ya watu wa Comoros na kudumisha utulivu.