UM na AU walaani shambulio la Sortoni Darfur wiki hii

UM na AU walaani shambulio la Sortoni Darfur wiki hii

Mwenye kiti wa tume ya Muungano wa Afrika , Nkosazana Dlamini-Zuma, Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa, Ban Ki-moon,wamelaani shambulio la mapema wiki hii lililofanywa na kundi la wanamgambo wenye silaha, kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani pia ufyatulianaji wa risasi karibu na soko mjini Sortoni Darfur Kaskazini.

Mashambulio hayo yamesababisha vifio vya watu watano , wakiwemo watoto wawili na kujeruhi watu wengine wengi akiwemo mlinda amani kutoka Ethiopia wa mpango wa pamoja wa Umoja wa mataifa na Muungano wa Afrika wa kulinda amani Darfur, UNAMID .

Mwenyekiti wa Au na Ban wameelezea hofu yao kufuatia kuongezeka kwa mvutano baina ya jamii za wafugaji wa kuhamahama na wakimbizi wa ndani katika eneo hilo la Darfur.

Wametoa wito kwa pande husika kujizuia na vitendo vya ghasia na kutatua tofauti zao kwa njia ya majadiliano. Pia wameitaka serikali ya Sudan kuchunguza na kuwafikisha haraka kwenye mkono wa sheria wahusika wa mashambulio hayo.