Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwandishi Florence Hartmann aachiliwa huru na mahakama ya kimataifa The Hague

Mwandishi Florence Hartmann aachiliwa huru na mahakama ya kimataifa The Hague

Rais wa mfumo uliorithi mahakama ya kimataifa ya uhalifu kwa Rwanda na Yugoslavia ya zamani, MICT ametangaza leo kumwachilia mapema mwandishi wa habari Florence Hartmann.

Katika taarifa iliyotolewa na MICT, rais huyo ameeleza kwamba uamuzi huo umechukuliwa kutokana na tabia nzuri ya Bi Hartmann kwenye kifungo chake na kwa sababu tayari ametimiza zaidi ya theluthi mbili ya kifungo alichohukumiwa.

MICT imesema pia kwamba Bi Hartmann ameishtaki mahakama hiyo akilalamikia mazingira ya kutengwa kizuizini kwenye kituo cha kizuizini cha Umoja wa Mataifa, MICT ikieleza kwamba malalamiko hayo hayakuwa na msingi.

Mwandishi huyo ambaye alikuwa msemaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa Yugoslavia ya zamani, TPIY, alikamatwa na kufungwa na MICT wakati akihudhuria utaoji hukumu dhidi ya kesi ya Radovan Karadzic, alhamis iliyopita.

Mwaka 2009, Bi Hartmann alikutwa na hatia ya kutoa siri za TPIY katika kitabu alichoandika kuhusu kesi ya Slobodan Milosevic na kuhukumiwa kifungo cha siku saba na faini ya euro elfu saba.