Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon alaani mashambulizi ya Cote d'Ivoire

Ban Ki-moon alaani mashambulizi ya Cote d'Ivoire

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea kwenye hoteli tatu za mji wa Grand-Bassam nchini Cote d'Ivoire, siku ya Jumapili, ambapo watu angalau 16 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wake imemnukuu Ban Ki-moon akituma salamu zake za rambi rambi kwa familia za wahanga, raia na serikali ya Cote d'Ivoire.

Akizungumza leo na waandishi wa habari, msemaji wa Katibu Mkuu Stéphane Dujarric ameongeza kwamba mfanyakazi mmoja wa kujitolea wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo ONUCI ameuawa katika mashambulizi hayo, na askari polisi mmoja wa ONUCI akijeruhiwa.

Kwa upande wake Baraza la Usalama pia limelaani vikali mashambulizi hayo yaliyodaiwa na kundi la kigaidi la AQMI.

Wanachama wa Baraza hilo wameeleza kuunga mkono juhudi za Cote d’Ivoire na nchi jirani katika kupambana na ugaidi, wakisisitiza umuhimu wa kuongeza jitihada za kikanda na kimataifa katika kupambana na ugaidi na itikadi kali na katili.