Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Angalau DPRK sasa inasikiliza Baraza la Haki- Balozi Choi

Angalau DPRK sasa inasikiliza Baraza la Haki- Balozi Choi

Rais wa Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa Balozi Kyong-lim Choi amesema kutokomeza ukiukwaji wa haki za binadamu huko Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK, Burundi na Syria ni miongoni mwa vipaumbele vya vikao vya baraza hilo vinavyoanza Jumatano ijayo.

Akihojiwa na Radio ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi, Balozi Choi ambaye ni mara ya kwanza anashika wadhifa huo amesema nchi hizo ni kati ya 47 zitakazoangaziwa utendaji wake wa haki za binadamu ambapo ukiukwaji wa haki unaleta majanga.

Hata hivyo amesema majanga yote yanayoendelea duniani hayawezi kutatuliwa  na taasisi moja pekee lakini ana uhakika baraza la haki za binadamu limekuwa na mafanikio, angalau kidogo tu kwenye janga la Syria..

“Nadhani tunapaswa kuelewa kuwa mijadala katika baraza la haki za binadamu ni sehemu ya juhudi za jamii ya kimatafia kusuluhisha mzozo wa Syria. Na pia tutapeleka ujumbe thabiti kwa watu wa Syria wanaotekeleza uhalifu huu ya kwamba  hatimaye watawajibika kwa vitendo vyao.”

Kuhusu DPRK, Balozi Choi ambaye yeye anatoka Korea Kusini amesisitiza kutoegemea upande wowote, huku akieleza kuwa kwa sasa angalau nchi hiyo ya Korea Kaskazini au DPRK imekuwa inatazama na kusikiliza kile kinachosemwa na baraza la haki.