Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban amelaani vikali shambulio la kigaidi Pakistan

Ban amelaani vikali shambulio la kigaidi Pakistan

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali shambulio la kigaidi la wanamgambo wenye silaha lililofanyika leo kwenye chuo kikuu cha Bacha Khan mjini Charsadda, Pakistan, na kuuwa watu 19 huku wengine wengi wakijeruhiwa.

Ban amesikitishwa na vitendo hivyo vya ghasia na kutoa wito wa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria wote waliohusika na ukatili huo.

Ban anakumbuka kwamba zaidi ya mwaka mmoja uliopita Pakistan ilikabiliwa na moja ya mashambulio mabaya kabisa shuleni katika historia mjini  Peshawar, ambapo watu zaidi ya 150 waliuawa wengi wakiwa ni watoto wa shule.Amerejea kusema mashambulio dhidi ya wanafunzi, walimu au shule asilani hayawezi kuhalalishwa.

Akiongeza kuwa haki ya elimu kwa wote ni lazima ilindwe, shule na majenge ya elimu lazima viheshimiwe na kutambulika kama ni maeneo salama. Ban ametaka hatua zichukuliwe kuhakikisha kwamba shule katika maeneo yasiyosalama na yenye vita zinalindwa ipasavyo.

Ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika, watu na serikali ya Pakistan kwa zahma iliyowafika.