Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Apu ya #ShareThe Meal yatimiza lengo lake

Apu ya #ShareThe Meal yatimiza lengo lake

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP limetangaza leo kwamba limefikia lengo lake la kuwapatia watoto wakimbizi 20,000 wa Syria waliopo Jordan mlo wa shuleni kwa mwaka mzima, kupitia mradi wake mpya wa apu ya simu za mkononi iitwayo “Share the Meal”.

Kwenye taarifa  iliyotolewa leo, WFP imesema kwamba sasa Share the Meal italenga watoto, wakinamama na wanawake wajawazito waliopo mjini Homs, Syria ili kuimarisha mlo wao na kuwapatia nyama, mazima, matunda na mboga mboga.

Kwa mujibu wa WFP, mlo wenye vyakula tofauti tofauti ni muhimu kwa afya ya mwanamke mjamzito na anayenyonyesha, pia katika siku 1,000 za kwanza za maisha ya mtoto.

Kupitia apu ya “Share the Meal”mtu yeyoye kote duniani anaweza kutoa msaada wenye thamani ya senti 50 za kimarekani, ambayo ni kiasi cha pesa kinachohitajika kila siku kusaidia mtu mmoja kupata chakula. Hadi sasa ni milo milioni 4 ambayo imefadhiliwa.