Hali ya kibinadamu Yemen yazidi kutia wasiwasi:OHCHR

Hali ya kibinadamu Yemen yazidi kutia wasiwasi:OHCHR

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, imeelezea masikitiko yake kutokana na kuendelea kwa mashambulizi ya anga kwenye maeneo ya raia, ikiwemo mashambulio yaliyoripotiwa leo asubuhi.

Hadi sasa ofisi hiyo imesema haijaweza kuthibitisha iwapo mashambulizi hayo ya leo yamesababisha vifo, lakini imeeleza kuwa idadi ya raia wanaouawa kutokana na mzozo unaoendelea nchini humo imefikia 2795 ambapo mwezi Disemba pekee idadi ilikuwa 81 na kuzidi mwezi uliotangulia wa Novemba.

Msemaji wa ofisi hiyo ya haki za binadamu huko Geneva, Uswisi, Rupert Colville amesema mashambulizi yanafanya na vikosi vya ushirika na kwamba wanasalia na hofu kubwa ya hali ya kibinadamu kwenye mji wa Taizz.

(Sauti ya bwana Colville)

“Mji huu umekuwa eneo la mapigano ya kutisha kwa miezi minane sasa bila kutulia. Udhibiti uko katika maeneo yote ya kuingia mji huu na unafanywa na kamati zenye ushirika na wahouthi na hivyo kukwamisha uwezo wa kufikisha mahitaji muhimu kama vile chakula. Hali inakuwa mbaya zaidi kwa raia na hali ya kiafya pia kwenye eneo hilo ni mbaya kwani hata hospitali kubwa pekee ya Al Rawdha imelazimika kusitisha huduma kwa wagonjwa.”

Halidhalika Bwana Colville amesema hali ya magereza huko Yemen inazidi kuathiriwa na mzozo kwani tangu mwezi Machi mwaka jana zaidi ya wafungwa 40 wameuawa na 10 wamejeruhiwa na makombora yanayorushwa kiholela.