Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kusimamishwa kwa NGOs Burundi ni hatua nyingine ya kunyamazisha jamii : Zeid

Kusimamishwa kwa NGOs Burundi ni hatua nyingine ya kunyamazisha jamii : Zeid

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Zeid Raád Al Hussein amelaani maamuzi ya mamlaka za serikali ya Burundi kusimamisha mashirika kumi yasiyo ya kiserikali (NGOs) zikiwemo baadhi ya zinazohusiana na maswala ya haki za binadamu, mateso na haki za wanawake na watoto.

Kwenye taarifa yake iliyotolewa leo, Bwana Zeid ameelezea wasiwasi wake akisema kwamba maamuzi hayo yanaendeelea kudhoofisha sauti ya jamii nchini humo, na kuhatarisha mafanikio ya mazungumzo jumuishi yanayotakiwa kuanza hivi karibuni, akiongeza kwamba inaweza kuwa dalili ya kuonyesha nia ya serikali ya Burundi ya kunyamazisha sauti za upinzani.

Aidha ameeleza kwamba vyombo vitano vya habari vilivyosimamishwa mwezi Juni mwaka huu havijaweza kuanza upya shughuli zao.

Kamishna Zeid amekariri kwamba mashirika yasiyo ya kiserikali yanapaswa kuendelea na shughuli zao bila kuzuiliwa. Ameongeza kuwa tangu mwezi April, viongozi 15 wa jamii wamelazimika kukimbia nchi, huku wengine 4 wakiwa wameuawa na polisi au wanamgambo.

Kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu, watu 277 wameuawa tangu mwezi April mwaka huu.