Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jeshi na polisi DRC watekeleza asilimia 60 ya ukiukaji wa haki za binadamu

Jeshi na polisi DRC watekeleza asilimia 60 ya ukiukaji wa haki za binadamu

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, visa 407 vya ukiukaji wa haki za binadamu vimeripotiwa mwezi uliopita wa Oktoba, imesema Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini humo. ambapo miongoni mwao, visa 21 vimehusishwa na mchakato wa uchaguzi.

Kwenye ripoti yake, ofisi hiyo imesema idadi hiyo imepungua ikilinganishwa na mwezi Septemba ambapo idadi ya kesi hizo ilikuwa ni zaidi ya 500, lakini hata hivyo mwelekeo unatia wasiwasi.

Aidha maandamano 7 ya vyama vya upinzani yamekataliwa au kufurushwa kwa ghasia, huku maandamano 11 ya chama tawala yakiendelea kwa amani.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kinshasa, mkuu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini DRC José Maria Aranaz amesema...

(Sauti ya bwana Aranaz)

“Kama kawaida majimbo yaliyoathirika zaidi ni majimbo ya mashariki. Wafanyakazi wa serikali wametekeleza asilimia 60 ya visa vya ukiukaji wa haki za binadamu viliyoripotiwa. Miongoni mwao ni jeshi waliotekeleza visa vingi wakifuatiwa na polisi na majasusi.”

Waasi wa FRPI, FDLR na LRA wamedaiwa kutekeleza asilimia 41 ya visa vya ukikakaji wa haki.