Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa vyoo wahatarisha zaidi maisha ya watoto:UNICEF

Ukosefu wa vyoo wahatarisha zaidi maisha ya watoto:UNICEF

Leo ikiwa ni Siku ya Choo Duniani, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, limesema kuwa ukosefu wa vyoo unahatarisha maisha ya mamilioni ya watoto maskini zaidi duniani, likionyesha uhusiano kati ya kukosa huduma za kujisafi na utapiamlo.

Watu wapatao milioni 2.4 duniani hawana vyoo, na mtu mmoja kati ya wanane huenda haja kubwa hadharani.

UNICEF inakadiria kuwa watoto wapatao milioni 159 chini ya umri wa miaka mitano wamedumaa huku wengine milioni 50 wakiwa wana uzani mdogo kuliko inavyotarajiwa.

Ripoti iliyotolewa leo na UNICEF, Shirika la Misaada la Marekani, USAID na Shirika la Afya Duniani, WHO, imesema kuwa kukosa huduma za kujisafi, hususan kuenda haja kubwa hadharani huchangia visa vya kuhara na kueneza minyoo, ambayo husababisha utapiamlo.