Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon apongeza Myanmar kwa uchaguzi wa kihistoria

Ban Ki-moon apongeza Myanmar kwa uchaguzi wa kihistoria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amewapongeza raia wa Myanmar kwa kushirikiana kwa amani kwenye uchaguzi wa kihistoria uliofanyika tarehe 8 Novemba.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, Bwana Ban amenukuliwa akimpongeza Daw Aung San Suu Kyi na chama cha National League for Democracy kwa ushindi wake kwenye uchaguzi huo akipongeza pia chama tawala na taasisi za jeshi kwa kukubalia matokeo hayo.

Katibu Mkuu ameongeza kwamba hayo ni mafanikio makubwa katika utaratibu wa mpito wa demokrasia nchini humo. Amepongeza Tume ya Uchaguzi, vyama vya kisiasa, wachunguzi wa kitaifa na kimataifa, na wote waliofanikisha uchaguzi huo uliokuwa wazi na huru, akitoa wito kwa kuendeleza hali ya utulivu nchini humo wakati ambapo uataratibu wa kuunda serikali mpya unaendelea.

Hata hivyo Bwana Ban amesikitishwa na kuona kwamba vikundi vya watu walio wachache kama vile jamii ya Rohingya wamekataliwa kupiga kura na hata kugombea nafasi za kuchaguliwa.

Amesema bado njia ni ndefu ili kuhakikishia uchaguzi ujao unawa jumuishi, na kukuza haki za binadamu nchini humo bila kubagua mtu yeyote.