UNAMID na jukumu la kuimarisha usalama kwenye kambi za wakimbizi

UNAMID na jukumu la kuimarisha usalama kwenye kambi za wakimbizi

Kaimu Kamishna wa Polisi kwenye ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika huko Darfur, UNAMID Dkt. Mutasem Almajali amesema kiwango cha mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi kwenye eneo hilo kimepungua katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Dkt. Almajali amesema hayo alipohojiwa na Radio ya Umoja wa Mataifa kando mwa vikao vya makamishna wa polisi kwenye operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Hata hivyo amesema wanachoshuhudia mara kwa mara hivi sasa ni ongezeko la mapigano ya kikabila na wanachofanya sasa ni kutathmini kuona kile ambacho wanaweza kufanya kupunguza msuguano huo lakini kuna kikwazo.

(Sauti ya Dkt, Almajali)

“Sasa hoja ya serikali ya Sudan kuwa hilo si mamlaka yetu, huo ndio msimamo wa kisiasa wa serikali ya Sudan, inasema hapana hilo si jukumu lenu.”

Dkt. Almajali akazungumzia pia kile wanachofanya kuimarisha ulinzi kwenye kambi za wakimbizi wa ndani ambazo UNAMID ina jukumu la kuhakikisha usalama.

(Sauti ya Dkt. Almajali)

“Tunajaribu kuweka mazingira ambayo yatapunguza matukio ya kila siku yanayosababisha hofu juu ya usalama. Miongoni ni vikao vya kamati za polisi jamii, polisi wa kujitolea, kuimarisha polisi jamii kwenye kambi za wakimbizi wa ndani na pia tunajaribu kuwaleta pamoja wakimbizi wa ndani na polisi jamii ili waelewane. Hii ni kwa sababu tuna kambi kadhaa za wakimbizi wa ndani ambako polisi jamii hawakubaliki.”