Skip to main content

UNAMA yalaani mauaji ya raia saba

UNAMA yalaani mauaji ya raia saba

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA umelaani mauaji yaliyotekelezwa  na kikundi hasimu wa serikali dhidi ya raia saba , wakiwamo wanawake wawili, msichana mmoja na mvulana mmoja huko kusini mwa jimbo la Zabul.

Raia hao saba walitekwa nyara mwezi uliopita na kuuliwa kati ya Novemba sita na nane katika wilaya iitwayo Arghandab wakati ambapo machafuko yaliripotiwa katika eneo hilo kati ya makundi mawili hasimu.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu na mkuu wa UNAMA Nicholas Haysom amenukuliwa akisema kuwa mauaji hayo hayakubaliki na kutaka wauaji wafikishwe katika vyombo vya sheria.

UNAMA imesisitiza kuwa kuuwawa kwa raia na utekwaji ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu ambazo zinapaswa kufuatwa na pande zote kinzani ikiwamo vikundi vilivyo kinyume na serikali. Ujumbe huo pia umetuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao.