Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wabunge Burundi msichochee chuki bali jengeni amani:IPU

Wabunge Burundi msichochee chuki bali jengeni amani:IPU

Wakati taarifa za mauaji raia zikiripotiwa kila uchao huko Burundi, Umoja wa mabunge duniani, IPU, umesema wabunge wana wajibu wa kuongoza harakati za kuleta amani na utulivu badala ya kuchochea ghasia na mgawanyiko miongoni mwa jamii. Priscilla Lecomte na maelezo zaidi.

 (Taarifa ya Priscilla)

Katibu Mkuu wa IPU Martin Chungong ametoa kauli hiyo kufuatia ghasia zinazoendelea nchini humo akigusia pia ripoti za mashambulizi dhidi ya vikundi vya upinzani.

Asema mhimili huo haupaswi kuangusha wananchi au kusahau wajibu wake wa kuwakilisha jamii wakati huu ambapo jamii ya kimataifa inasalia na wasiwasi mkubwa kwa hali inayoendelea nchini humo.

Bwana Chungong amesema baada ya mazingira ya hofu kufuatia mzozo wa kisiasa uliosababisha mamia ya watu kuuawa na wengine kupoteza makazi, wabunge wanapaswa kuwa sehemu ya suluhu la mzozo baada ya tatizo.

Akizungumza na redio ya Umoja wa Mataifa leo, Bwana Chungong amewaomba wabunge washirikiane ili kurejesha maridhiano.

(sauti ya bwana Chungong)

" Wabunge ni viongozi wa maoni ya jamii, wana jukumu kubwa kimaadili. Wanapaswa kwenda kwenye mitaa ya mji wa Bujumbura ili kuzungumzia amani. Pia wanapaswa kuongea na mamlaka za  serikali ili waandae harakati za mazungumzo jumuishi."