Skip to main content

Ban Ki-moon atoa wito kwa Mashariki ya Kati

Ban Ki-moon atoa wito kwa Mashariki ya Kati

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema leo kwamba iwapo ghasia zitaendelea Mashariki ya Kati kwa misingi ya kidini, huenda itafika hatua ya kutoweza kudhibitika tena.

Amesema hayo akizungumza leo na waandishi wa habari, baada ya ziara yake kwenye eneo hilo ambapo amekuwa na mazungumzo na Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas, na viongozi wa Israel akiwemo Wazir Mkuu Benjamin Netanyahu na Mfalme Abdulah wa Jordan pamoja na familia za wahanga wa mashambulizi ya siku chache zilizopita.

Akieleza kushtushwa sana na kiwango cha mvutano kwenye maeneo ya Palestina hasa mjini Jerusalem, Bwana Ban ametoa wito kwa pande zote zijizuie kutumia aina yoyote ya ghasia, akisema

(Sauti ya bwana Ban)

“ Kitendo kimoja cha kuua au kubomoa nyumba kinasababisha hasira ya familia nzima. Msiba moja unasambaza hasira kwa maelfu. Nguvu za jeshi zinapaswa kutumiwa mwishoni siyo mwanzoni. Harakati za kiusalama hazitasitisha ghasia.”

Aidha ameongeza kwamba ili kufikia suluhu ya mataifa mawili lazima pande zote mbili zikubali kulegeza misimamo yao akikariri umuhimu wa kuunda taifa huru kwa wapalestina na kusitisha utawala wa Israel.

Hatimaye amesema, licha ya chuki na hasira, bado fursa ipo ya kurudi nyuma na kuzuia hatari ya vita.