Mtaalam wa UM ahofia hatma ya wakimbizi wa ndani Darfur

Mtaalam wa UM ahofia hatma ya wakimbizi wa ndani Darfur

Mtaalam mpya wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Sudan, Aristide Nononsi, ametoa wito kwa serikali ya Sudan na jamii ya kimataifa kuweka na kuendeleza mazingira salama kwa jamii za wakimbizi wa ndani Kaskazini na Kusini mwa Darfur.

Bwana Nononsi amesema baada ya kuzuru kambi za wakimbizi wa ndani Kaskazini na Kusini mwa Darfur hivi karibuni, ametiwa wasiwasi, sio tu na watu kuendelea kufurushwa makwao pamoja na tatizo la kibinadamu linalozuka, bali pia na hatma ya wakimbizi hao.

Amesema ingawa kambi hizo za wakimbizi hupokea usaidizi kutoka kwa serikali na mashirika ya Umoja wa Mataifa, ni muhimu kuona kuwa vitendo hivyo vinakwenda sambamba na haki za raia, na kuona njia za kuvifanya endelevu. Ametoa wito wakimbizi wa ndani wanaoishi katika hali mbaya wasaidiwe, pamoja na kushughulikia haki zao za kiuchumi, kijamuu na kitamaduni.