Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yakaribisha hatua ya Myanmar kupokea wahamiaji waliokwama baharini

UNHCR yakaribisha hatua ya Myanmar kupokea wahamiaji waliokwama baharini

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limekaribisha uamuzi wa serikali ya Myanmar kupokea watu 200 waliokuwa wamekwama kwenye bahari karibu na jimbo la Rakhine.

Watu hao wamepokelewa na UNHCR kwenye kituo kipya cha mapokezi kilichoandaliwa kwa ushirikiano na serikali ya Myanmar na tayari wamepewa usaidizi wa dharura,

Kwa mujibu wa Adrian Edwards, msemaji wa UNHCR, bado watu 2,000 wamekwama kwenye bahari karibu na Myanmar, wengine 1,500 wakiwa kusini zaidi kwenye bahari ya Andaman.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Geneva, msemaji huyo amesisitiza umuhimu wa kuwasaidia watu hao na kuwawezesha kushuka kwa boti.

Halikadhalika amesema kufuatia tangazo la Indonesia, Malaysia na Thailand la kuwasaidia watu waliokwama baharini, UNHCR inashirikiana na serikali hizo ili kuimarisha msaada unaotolewa.

Nchini Indonesia, zaidi ya watu 1,800 kutoka jamii ya Rohingya na Bangladesh wameshapokelewa tangu Mei,10, wengine 1,100 wakiwa wamefika Malaysia.