Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Robert Piper ateuliwa kuwa naibu mratibu wa mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati

Robert Piper ateuliwa kuwa naibu mratibu wa mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametangaza uteuzi wa Robert Piper wa Australia kama Naibu mratibu wa mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati katika ngazi ya msaidizi wa Katibu Mkuu.

Bwana Piper pia atafanya kazi kama mratibu mkazi na mratibu wa masuala ya kibinadamu kwenye eneo linalokaliwa la Palestina.

Bwana Piper atachukua nafasi ya James Rawley wa Marekani ambaye Ban amemshukuru sana kwa kazi yake na hususani mchango wake mkubwa katika juhudi za ujenzi wa Gaza.

Bwana Piper ana uzoefu wa miaka zaidi ya 25 katika masuala ya kibinadamu na maendeleo kwenye Umoja wa mataifa, akiongoza juhudi za ujenzi wa amani, kuzuia migogoro na upunguzaji wa majanga katika hali mbalimbali.

Piper amekuwa Mratibu wa Umoja wa mataifa wa masuala ya kibinadamu katika ukanda wa Sahel tangu mwaka 2013. Na kuanzia mwaka 2008 hadi 2013 alikuwa mratibu mkazi wa shirika la Umoja wa mataifa la maendeleo UNDP nchini Nepal na kabla ya hapo alifanya kazi kama hiyo Kosovo kati ya 2000 na 2004.

Bwana Piper ana shahada ya Sanaa na siasa kutoka chuo kikuu cha taifa cha Australia, alizaliwa mwaka 1966, ana mke na watoto wanne.