Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yaanza kampeni ya dharura ya chanjo kwa maelfu ya watoto walio hatarini Nepal

UNICEF yaanza kampeni ya dharura ya chanjo kwa maelfu ya watoto walio hatarini Nepal

Watoto zaidi ya nusu milioni wanalengwa katika kampeni ya dharura ya chanjo nchini Nepal wakati hofu ikiongezeka ya mlipuko wa surua kwenye makambi yasiyo rasmi yalianzishwa tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi nchini humo April 25.

Kampeni hiyo imezinduliwa na wizara ya afya na idadi ya watu ya Nepal kwa msaada wa shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na shirika la afya duniani WHO.

Mashirika hayo ynasema ukosefu wa malazi na usafi ni sababu kubwa ya hatari ya kuzuka maradhi wakati idadi ya watu waliozikimbia nyumba zao ikiendelea kuongezeka na wengi wao sasa wanaishi karibu na nyumba zao ambazo zimebomolewa kabisa na tetemeko.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa kabla ya tetemeko nchini Nepal mtoto mmoja kati ya 10 hajapatiwa chanjo ya surua. Tomoo Hozumi ni mwakilishi wa UNICEF Nepal

(SAUTI YA TOMOO HOZUMI)

“Mengi yamefanyika lakini zaidi yanahitajika kwa haraka. Katika siku zjazo, shule zinapaswa kufunguliwa upya haraka iwezekanavyo ili kurahisisha watoto kupona kiwewe. Watoto waliopoteza wazazi wao wanahitaji kuhudumiwa ipasavyo ili kuzuia hatari za ukatili au biashara haramu” 

Takriban watoto milioni 1.7 wanahitaji msaada wa haraka katika maeneo yaliyoathirika Zaidi na tetemeko nchini Nepal.