Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Michael Douglas atambua umuhimu wa utafiti katika kupambana na tishio la nyuklia

Michael Douglas atambua umuhimu wa utafiti katika kupambana na tishio la nyuklia

Kongamano la kutathmini mkataba wa kuzuia ueneaji wa silaha za nyuklia, NPT, likiendelea leo mjini New York, mcheza filamu mashuhuri Michael Douglas ambaye pia ni Mjumbe wa Amani wa Umoja wa Mataifa amesema utafiti ni muhimu ili kutokomeza tishio la silaha za nyuklia.

Ameeleza kwamba yeye mwenyewe ameishi wakati wa tishio la silaha hizo kwenye vita baridi ambapo wakati wa utoto wake alikuwa anajificha chini ya dawati lake kwa hofu ya silaha hizo.

Ameongeza kwamba silaha za nyuklia bado ni tishio kubwa kwa binadamu na mazingira.

“ Idadi ya silaha za nyuklia duniani imepungua kwa zaidi ya nusu tangu wakati wa kilele cha vita barird. Lakini tishio la silaha za nyuklia bado halijapungua tangu wakati wa udogo wangu. Hata kama idadi ya silaha imepungua, silaha hizo na jinsi ya kuzitumia zina nguvu zaidi na za kisasa kuliko zamani”

Amesisitiza umuhimu wa utafiti katika kubuni njia mbadala ya matumizi ya silaha za nyuklia na kuongeza uelewa kuhusu swala hilo.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Uholanzi Bert Koenders amekariri nguzo tatu za mkataba wa kuzuia ueneaji wa silaha za nyuklia zikiwa ni kuondoa silaha za nyuklia, kuzuia ueneaji wa silaha hizo na kuendeleza matumizi ya kawaida ya nyuklia.

Amesema mkataba huo ni msingi wa amani ya kimataifa, akifurahia na mafanikio yaliyopatikana licha ya mvutano na changamoto zinazokumba utekelezaji wa mkataba huo.