Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laongeza muda wa MINUSCA

Baraza la Usalama laongeza muda wa MINUSCA

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limepitisha kwa kauli moja azimio la kuongeza kwa mwaka mmoja zaidi muda wa mamlaka ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, MINUSCA.

Katika azimio hilo wanachama wa baraza la usalama wamesisitiza umuhimu wa kuendeleza utaratibu wa mpito, hasa kuisaidia serikali ya CAR katika kongamano la maridhiano la Bangui litakalofanyika wiki ijayo na katika maandalizi ya uchaguzi unaotakiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Aidha wameeleza wasiwasi wao kuhusu hali ya usalama ambayo inazidi kuwa tete licha ya kuimarika kwenye baadhi ya maeneo na hivyo wameamua kutopunguza idadi ya walinda amani na polisi wa MINUSCA ambayo ilikuwa imeongezwa hadi wanajeshi 10,000 na polisi 2,000.

Halikadhalika wanachama wa baraza hilo wameongeza mamlaka za MINUSCA katika maswala ya kuhakikisha usalama nchini humo, kulinda haki za binadamu na hasa kwa watoto na kuboresha mamlaka za serikali kwenye wakati wa mpito.

Kwa mujibu wa ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ni watu milioni 2.7 wanaoripotiwa kuhitaji usaidizi wa kibinadamu nchini humo, na zaidi ya 400,000 ni wakimbizi wa ndani.