Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban awaomba viongozi wa Kiarabu kupambana na misingi ya ugaidi

Ban awaomba viongozi wa Kiarabu kupambana na misingi ya ugaidi

Nchi za Kiarabu zinahitaji kuimarisha utawala wa sheria, kuheshimu haki za wanawake na binadamu wote kwa ujumla ili kufikia utulivu endelevu wa kisiasa.

Hii ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akihudhuria mkutano wa muungano wa nchi za kiarabu, mjini Sharm el-sheik, Misri.

Amewasihi viongozi wa Kiarabu waongeze ushirikiano wao kwa ajili ya usalama wa raia wa ukanda huo na wa dunia nzima, akiongeza kwamba vita, ghasia, ugaidi na kukaliwa kwa Palestina na Israel vinasababisha mateso mengi.

Amesema kwamba ni lazima kukabiliana na misingi ya misimamo mikali, akiongeza kwamba ni lazima kuheshimu haki za binadamu wakati wa kupambana na misimamo mikali katili.

Kuhusu Syria, Ban amesema anasikia hasira na aibu, akieleza hasira zake zinatokana na uharibifu wa Syria na aibu yake kutokana na kushindwa kwa jamii ya kimataifa kukomesha mauaji ya raia wa Syria.