Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Haki za Binadamu kujadili ukiukwaji wa Boko Haram

Baraza la Haki za Binadamu kujadili ukiukwaji wa Boko Haram

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, limetangaza leo kuwa litafanya kikao maalum mnamo Aprili mosi kuhusu ukiukwaji unaotekelezwa na kundi la Boko Haram.

Hatua hiyo inafuatia ombi la ujumbe wa Algeria kwa niaba ya wawakilishi wa Afrika kwenye Baraza hilo, ambalo liliwasilishwa kwenye sekritariati ya Baraza mnamo Alhamis jioni.

Hapa, ni Rais wa Baraza la Haki za Binadamu Joachim Ruecker akitoa tangazo hilo.

“Ningependa kukuelezeni kuwa nimepokea barua mnamo Machi 26 2015 saa kumi na mbili kasoro dakika tano, kutoka kwa Balozi wa Kudumu wa Algeria, ikiwa na ombi la kuitisha kikao maalum cha Baraza hili, na nanukuu, kutokana na mashambulizi ya kigaidi na ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram, mnamo Jumatano, Aprili mosi, mwaka 2015.”

Wanamgambo wa Boko Haram wamekuwa wakifanya mashambulizi mara kwa mara kaskazini mashariki mwa Nigeria na katika nchi jirani, ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwalazimu makumi ya maelfu ya wengine kuhama makwao, wakikimbilia nchi za Chad, Cameroon na Niger.