Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio la nafasi ya mtaalamu wa haki za albino lapitishwa Geneva

Azimio la nafasi ya mtaalamu wa haki za albino lapitishwa Geneva

Katika kuhakikisha vitendo dhalimu dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi albino ikiwamo mauaji na ubaguzi vinatokomezwa Umoja wa Mataifa umepitisha azimio la kuanziswha kwa nafasi ya mtaalamu maalum kuhusu haki za kundi hilo atakayechunguza ukatili dhidi ya albino na kukuza usawa.Katika kikao cha 28 cha baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kinachoendelea mjini Geneva kimekuwa kikifuatilia matukio dhidi ya albino barani Afrika kikisema watoto na hata watu wazima wameathiriwa pakubwa hususani Afrika Mashariki ambapo viungo vyao huuzwa kwa imani za kishirikina.

Zikiongozwa na ujumbe wa Algeria nchi za Afrika kwa kushirikiana na nchi nyingine 21 zimewasilisha pendekezo hilo kwa baraza la haki za binadamu na kusema mtaalamu huyo mpya au mtaalamu maalum atatoa mrejesho kuhusu vikwazo na changamoto zinazowakumba watu wenye ulemavu.

Azimio hilo linampa mamalaka mtaalamu huru au maalum , kushirikiana na nchi na wadau wengine husika katika kuhakikisha haki za albino huku pia likitoa muda wa miaka mitatu kufanya kazi na mataifa ambapo mashambulizi dhidi ya albino yametekelezwa.

Nchi zilizotajwa katika mateso dhidi ya abino ni Tanzania, Malawi, na Burundi ambapo kumekuwa na taarifa za hivi karibuni za ukiukwaji wa haki za binadamu kwa watu wenye ulemavu wa ngozi, albino.