Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Cote d’Ivoire iendelee na jitahada zake inapoelekea uchaguzi

Cote d’Ivoire iendelee na jitahada zake inapoelekea uchaguzi

Jitihada za Côte d’Ivorie katika kurejesha usalama, kuimarisha sekta ya sheria na kusalimisha waasi zinapaswa kuendelea, wakati ambapo nchi hiyo inaelekea uchaguzi wa rais mwezi wa Oktoba mwaka huu amesema mtalaam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu uwezeshaji wa uwezo wa Cote d’Ivoire, Mohammed Ayat.

Amesema hayo katika mjadala uliofanyika leo mjini Geneva, Uswisi kwenye Baraza la Usalama ukimulika mafanikio yaliyopatikana katika kuboresha mfumo wa sheria, ikiwemo kuondoa adhabu ya kifo, na kutokomeza ukwepaji wa sheria.

Aidha Bwana Ayat amekaribisha uundwaji wa mfuko wa kufidia wahanga wa mzozo wa mwaka 2010 na 2011.

Hata hivyo, mtalaam huyo ametaja changamoto zinazobaki nchini humo, ikiwemo kujisalimisha kwa waasi ambao bado ni 30,000 nchini humo na kupambana na ukatili wa kijinsia unaokumba wasichana na wanawake.

Hatimaye Bwana Ayat ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuendelea kuisaidia Côte d’Ivoire, ambayo inaweza kuwa na jukumu la msingi la kurejesha utulivu katika ukanda wa Afrika Magharibi.