Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya usalama yazorota nchini Mali : Mtalaam wa UM

Hali ya usalama yazorota nchini Mali : Mtalaam wa UM

Nchini Mali, hali inazidi kuwa tete kutokana na vitisho vya usalama kutoka kwa waasi wanaotaka kuweka dola la uislamu wenye msimamo mkali na wale wanaotaka uhuru wa maeneo ya kaskazini mwa Mali ambao wamekuwa wakipigana na serikali ya Mali tangu 2012.

Hii ni kwa mujibu wa mtalaam maalum kuhusu haki za binadamu nchini humo, Suliman Baldo, ambaye amewasilisha leo ripoti yake mbele ya Baraza la Haki za Binadamu, mjini Geneva, Uswisi, akisitishwa na uamuzi wa vikundi hivyo vya waasi kutoheshimu sitisho la mapigano lililosainiwa mjini Algiers.

Mtalaam huyo amezingatia umuhimu wa kufikia makubaliano ya amani kati ya serikali ya Mali na waasi wanaopigania uhuru wa maeneo ya kaskazini.

"Kufikia makubaliano ya amani kutawezesha Umoja wa Mataifa, jamii ya kimataifa na serikali ya Mali kulipa kipaumbele tatizo la waasi wenye msimamo mkali wa kidini na wagaidi ambao wanaendelea na shughuliki zao kwenye eneo hilo, ajenda yao ikivuka mipaka ya Mali, na wakifaidika na hali ya Mali kutokuwa na amani na kuendelea vita. Wanaendelea na shughuli zao, wanafaidika na hali hiyo, lakini Wamali kwa kweli hawafaidiki »

Aidha Bwana Baldo ameeleza kwamba hali hiyo inaathiri usalama wa raia na haki za binadamu, ikiwemo haki ya kupata elimu, akiongeza kwamba zaidi ya theluthi moja ya shule zimefungwa tangu mwaka 2012.

Hatimaye amesikitishwa na mashambulizi yaliyotokea dhidi ya walinda amani wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, ambao mara kwa mara wanalengwa na mashambulizi kadhaa yakiwemo mabomu, makombora na mabomu ya kutegwa ardhini ambayo yanaathiri pia raia wa Mali.