Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yajikita katika kupambana na kipindupindu Malawi

UNICEF yajikita katika kupambana na kipindupindu Malawi

Nchini Malawi, ugonjwa wa kipindupindu uliolipuka kusini mwa nchi umesababisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF kuchukua hatua kwa dharura.

Msemaji wa UNICEF Christophe Boulierac amesema tayari visa 39 vimeripotiwa na wizara ya afya na watu wawili wamefariki dunia, kwenye kambi za wakimbizi wa ndani waliokimbia makwao baada ya mafuriko ya mwezi Januari.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva msemaji wa UNICEF amesema usipotibiwa, ugonjwa wa kipindupindu unaweza kumuua mtu kwa muda mfupi.

"Wakimbizi wa ndani wamo hatarini zaidi ya kuambukizwa, hasa wale ambao wamedhoofika sana, kama mfano watoto walioathirika na utapiamlo. Kutokana na mafuriko, huduma za afya nchini Malawi zimezidishwa tayari, lakini usambazaji wa kipindupindu ukiendelea kwa kasi, itakuwa ni shida kuutokomeza, pamoja na shida iliyopo bado ya kufikia watu »

UNICEF na wadau wake wanaisaidia serikali ya Malawi kupitia usambazaji wa vifaa vya matibabu na mahema, na vituo vidogo vya afya ili kuhudumia watoto walioathirika na utapiamlo.

Aidha msemaji huyo wa UNICEF amesema upatikanaji wa maji safi ni muhimu na kwa hivyo tayari watu 78,000 wamepatiwa huduma za maji na UNICEF.